MASOMO YA MISA DOMINIKA YA 4 YA PASAKA MWAKA C WA KANISA.
MASOMO YA MISA DOMINIKA YA 4 YA PASAKA(DOMINIKA YA KRISTO MCHUNGAJI MWEMA).
SIKU YA KUOMBEA MIITO
SOMO 1
Mdo 13:14, 43-52
Paulo na Barnaba walitoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.
Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana.
Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.
Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.
Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 100:1-3,5
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yo
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)
Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SOMO 2
Ufu. 7:9, 14b-17
Wakati ule, mimi, Yohane, niliona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.
Mmoja wa wale wazee akiniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 10:27-30
Yesu alisema; Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.
--------------------------------------------------------------------------
TAFAKARI (Sehemu ya Kwanza)
MUNGU ANATAKA WATU WOTE WA ULIMWENGU TUFIKIWE
Masomo tuliyosomewa yanatuambia jambo hili. Mpango wa Mungu wa kutukomboa wanadamu ni mpana. Ni mpango uliokusudiwa kuwafikia hata wanaoukataa. Injili inasema, watu wakishaupokea mpango huo wanapewa uzima wa milele na kuhakikishiwa ulinzi wasipotee. Yesu anasema yeye hupaswa kuwajibika kwa watu hao ili wasipokonywe mkononi mwake. Kwa kweli wako mkononi mwa Mungu Baba kwa vile Mungu Baba na yeye ni wamoja. Maneno haya ni ya faraja kubwa kwa mfuasi wa Yesu anayejitambua.
Hata hivyo, maelezo haya ya Injili yanaelekea kueleweka kana kwamba wanaokuwa Wakristo hawawezi kuingia jehanamu. Si sawa kuelewa hivyo kwa maana ijapokuwa ni kweli hakuna anayeweza kuwapokonya watu hao kutoka mikononi mwa Mungu, wanadamu kwa akili na utashi wao huweza kuamua kujidondosha kutoka mikononi mwa Yesu. Aidha kwa kumsikiliza Shetani humwasi Yesu na kumsaliti. Humkataa. Hapo ndipo huziweka roho zao rehani. Ndipo hao wataajibika kwa kujipoteza wenyewe. Lakini basi, kwa ujumla, wenye kujituliza na kujidumisha mikononi mwa Mungu hukaa salama salimini.
Somo la kwanza linasimulia mkasa wa Wayahudi kuikataa Injili. Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume anasimulia mambo yalivyokuwa. Anasema Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Ndipo Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa na kuwasikitikia wakisema, “Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwao kwanza; kwa kuwa wanalisukumia mbali, na kujiona nafsi zao kuwa hawastahili uzima wa milele basi wanawageukia watu wa Mataifa.” Mkasa huu ulisikitisha lakini ndio unadhihirisha pia kwamba Mungu anataka, kwa heri au kwa shida, watu wote wafikiwe na kutangaziwa Habari Njema ya furaha.
Somo la pili linatupa picha ya mambo yatakavyoishia huko mwishoni mwa historia. Linasema mradi utafanikiwa. Watu watapatikana na kufanya mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu atakayeweza kuuhesabu. Watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, watasimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wakiwa wamevikwa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Mungu atawatandia hema yake juu yao nao hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Somo linasema mambo yatakuwa hivyo kwa sababu Yesu, ndiye Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao. Hata hapo mradi wa watu wote kutakiwa kufika na kukaa na Mungu utakuwa umefanikiwa. Hata hivyo wale waliikataa Injili kama hawatakuwa wamejirudi watakuwa wamelipata walilolitafuta maana mwana kulitafuta mwana kulipata. Watakuwa wamejidondosha wenyewe kutoka mikononi mwa Kristo na kujipeleka wenyewe kwenye moto wa milele alioandaliwa Shetani na watu wanaomshabikia kama wao. Jambo hili la mwisho hatutaki litukute. Mungu tusaidie.
SALA
Ee Mungu mwenyezi mpango wako wa kutufikia watu wote tunauelewa pole pole. Tunakuomba utakapoukamilisha kabisa mbinguni, sisi nasi tuwemo kati ya uliowakusanya kwa uzima wa milele. Amina.
TAFAKARI (Sehemu ya Pili)
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu la Mwanza
SOMO LA KWANZA: Mdo. 13:14, 43-52
Jukumu la kuhubiri ufalme wa Mungu halikukoma baada ya Yesu kupaa mbinguni bali liliendelezwa na mitume pamoja na washirika wao wakimemo Paulo na Barnaba. Paulo na Barnaba wanapoendeleza kazi ya kumhubiri Kristo wanapata ufanisi mkubwa kwani idadi ya waamini inaongezeka sana. Hata hivyo, palipo na mafanikio hapakosi changamoto. Kuongezeka kwa idadi ya waamini kuliwafanya Wayahudi wasioamini waone wivu na hivyo kuanza kupindisha/kupotosha/kupinga mafundisho yaliyofundishwa na mitume juu ya habari za Kristo na hata kuwafitinisha mitume na watu wengine. Ukengeufu huu wa Wayahudi (kukataa Habari Njema ya wokovu kwa njia ya Kristo na kupotosha Neno la Mungu) kuliwafanya mitume kuelekeza zaidi nguvu zao kuwahubiria Injili “watu wa mataifa” (yaani watu ambao si Wayahudi, wapagani). Watu wa mataifa, baada ya kuhubiriwa, waliamini Habari Njema ya wokovu kwa furaha kubwa na kisha kuongoka.
Kutoka kwenye somo letu la kwanza tunajifunza mambo makubwa mawili: (1) Tunapokataa kulipokea Neno la Mungu, neema hiyo wanapewa watu wengine. Wayahudi walikuwa ni watu wa taifa teule la Mungu. Mungu alipenda habari ya wokovu ianzie kwao. Hata hivyo, kwa kuwa wengi wao walikataa kuipokea habari hiyo ya wokovu, Mungu aliamua kuwapa fursa hiyo watu wa mataifa mengine: _“… kwa kuwa mnalisukumia mbali [Neno la Mungu], angalieni, twawageukia Mataifa.”_ Kwa ufupi, Wayahudi hawakuwa tayari kupokea habari njema ya wokovu katika Kristo. Sisi nasi kwa ubatizo wetu tumefanywa kuwa taifa teule la Mungu. Hata hivyo, sisi ambao ni taifa teule la Mungu tukishindwa kupokea Habari Njema ya wokovu tutambue kwamba watapewa watu wengine, tena ambao tunawaona kama hawastahili kupata wokovu. Tutambue kuwa wokovu si mali ya watu wachache bali ni haki ya wote walio tayari kulipokea Neno la Mungu na kuongokea maisha mapya. Kwa bahati mbaya wengi wetu hatuna tofauti na Wayahudi wasioamini kwani nasi tunalisukumia mbali Neno la Mungu kwa namna mbalimbali: *kwa kutoona umuhimu na uzito wa kusoma Neno la Mungu, kwa kutoshika maagizo na mausia yaliyomo kwenye Neno la Mungu, kwa kutoona umuhimu wa kuishi maisha ya Sakramenti, n.k. Haya yatafanya tupoteze fursa ya kuupokea uzima wa milele. (2) Tujihadhari na watu wanaopotosha/wanaopinga Neno la Mungu. Somo letu linatuambia kuwa Wayahudi, baada ya kuona mahubiri ya mitume yanazaa matunda, _“walijaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.”_ Hapa tunajifunza kuwa tangu nyakati za mwanzo za Ukristo wapo watu ambao wanapotosha/wanalipinga/wanakanusha Neno la Mungu ama kwa sababu ya wivu au kwa sababu ya maslahi binafsi. Hata leo wapo watu wanaopotosha Neno la Mungu kwa sababu zao binafsi. Hawa ni “Wakristo wa uongo” ambao ndani yao kuna “manabii wa uongo” wanaokanusha Injili halisi ya Kristo: wanaahidi utajiri kwa wafuasi wao, wanahubiri injili ya miujiza (vipofu wataona, viwete watatembea na wafu watafufuliwa), wanaahidi kuwaondolea watu shida na mateso yao yote. Hawa wamesahau kuwa shida na mateso ni sehemu ya Injili ya Kristo ambaye naye pia aliteswa, alikufa na kufufuka. Tafakari, chukua hatua.
SOMO LA PILI: Ufu. 7:9, 14b-17
Somo letu la pili linatufunulia ujumbe kuwa “tukiwa mashuhuda waaminifu wa imani yetu tutashiriki utakatifu wa Mungu Baba.” Ili kuelewa somo letu la pili ni vizuri kurejea karne ya kwanza ya ukristo. Kuwa Mkristo katika karne ya kwanza haikuwa jambo rahisi kwani ukristo ulipata upinzani kutoka pande kubwa mbili: kutoka kwa utawala wa Kirumi (Wapagani) na kutoka upande wa Wayahudi ambao waliutazama ukristo kama tishio kwa imani ya Kiyahudi. Hivyo, Wakristo wengi walikamatwa na kufungwa gerezani, kupigwa mijeledi na hata kuuawa. Haya yote ndiyo yanaitwa madhulumu dhidi ya Wakristo (persecutions of the Christians). Kutokana na hali hii, wapo baadhi ya Wakristo waliikana imani yao ili kuokoa uhai wao na wapo Wakristo ambao walikuwa tayari kufa kwa ajili ya imani yao kwa Kristo. Maono anayoyapata Yohane yanalenga kuwatia moyo na kuwaimarisha Wakristo wanaoteseka kwa sababu ya imani yao na hivyo kuwahimiza kubaki waaminifu katika imani na hata ikiwapasa kufa kwani kwa kufa kwao hawatapata hasara yoyote kwa kuwa watapata tuzo mbinguni. Maono haya yanalenga kuwaambia Wakristo wanaoteseka kuwa: _wasiogope kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo (ndiko kufua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo) kwa kuwa wenzao waliokubali kufa kwa ajili ya Kristo wapo mbele za Mungu kwenye furaha isiyoelezeka kwani huko hawateseki tena kwa namna yoyote._ Kigezo kilichowafanya wawe mbele ya Mungu na kupata furaha ni hiki: wamekuwa mashuhuda waaminifu kwa Kristo licha ya dhiki ile iliyo kuu waliyopitia duniani. Hivyo, fundisho kuu la somo letu la pili ni hili: _tukiwa mashuhuda waaminifu wa imani yetu kwa Kristo, hasa tunapokumbana na mateso/dhiki, tutashiriki utakatifu wa Mungu Baba huko mbinguni._
Kile kilichokusudiwa katika maono anayoyapata Yohane katika somo letu la Pili ndicho Mungu anachokusudia kutufunulia leo. Yale tunayokumbana nayo hapa duniani kwa sababu ya imani yetu kwa Kristo yasiwe sababu ya sisi kuikana/kuiasi imani yetu bali tubaki waaminifu katika imani yetu kwa Kristo tukifahamu wazi kuwa ushuhuda imara wa imani yetu utatuwezesha kusimama mbele ya Mungu na kufurahia ushindi wetu dhidi ya uovu, changamoto, mateso na dhuluma za ulimwengu huu (matawi ya mitende yanayotajwa katika somo letu ni ishara ya furaha ya ushindi). Kila mmoja wetu ajiulize: je, dhiki kuu ya ulimwengu huu inakufanya uishi imani yako au inakufanya uikane imani yako? Ikiwa dhiki/mateso ya ulimwenguni huu inakufanya kuwa imara zaidi katika imani, basi hakika utashiriki utukufu wa Mungu/Kristo. Hakuna anayeingia mbinguni bila kupitia dhiki/mateso hapa duniani na anayekataa au kukwepa dhiki/mateso ya hapa dunia, anakataa/anakwepa mbingu. Tukabiliane na mateso, changamoto na dhuluma kwa jicho la imani ili hatimaye tupate furaha mbinguni ambapo Kristo Mwana-kondoo atafuta machozi yetu yote yatokanayo na mateso, changamoto na misiba tunayopitia.
SOMO LA INJILI: Yn. 10:27-30
Kabla ya kutafakari injili yetu ya leo ni vizuri kurudi na kusoma aya zinazotangulia somo letu la leo ili kujua mazingira ya somo lenyewe. Yesu, kama Myahudi mwingine yeyote, yupo hekaluni ili kusheherekea Sikukuu ya Kutabaruku (hii ilikuwa ni Sikukuu ya Kiyahudi ya kukumbuka tukio la kutakaswa na kuwekwa wakfu wa hekalu la Yerusalemu baada ya kuwa limenajisiwa na mfalme mpagani aitwaye Antioko Epifani, rejea 1 Makabayo 1:20-28; 41-61). Ni wakati wa sikukuu hii ndipo Wayahudi wanamfuata Yesu hekaluni na kumwambia, _“Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi” (rejea Yn. 10:24)._ Yesu anawajibu kuwa alikwishawaambia kuwa Yeye ndiye Kristo lakini hawakusadiki. Na kwa kuwa hawakusadiki, basi wao si sehemu ya kondoo wake (yaani wamekataa kumwamini na kuwa sehemu ya wafuasi wake). Wale waliomwamini ndio kondoo wake. Toka hapo Yesu anaanza kueleza sifa walizonazo kondoo wake na namna Yeye mchungaji Mwema anavyowatunza kondoo wake. Na ndipo inapoanzia Injili yetu ya leo.
Katika Injili ya leo Yesu anazungumzia sifa za kondoo wake na namna Yeye mwenyewe anavyowatunza. Kwanza, tuanze kuangalia sifa za kondoo wa Kristo: _(i) wanaisikia sauti ya mchungaji wao: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu.”_ Sauti ya Kristo Mchungaji Mwema ni ipi? Ni mafundisho anayofundisha Kristo. Kwa ufupi, sauti ya Kristo ni Habari Njema aliyoleta Kristo. Wale ambao ni kondoo wa Kristo daima wanasikia mafundisho ya Kristo, kuyaamini na kuyafanyia kazi ili mwishoni wapate uzima wa milele. _(ii) wanamfuata mchungaji wao._ Kumfuata mtu ni kuwa nyuma yake na kufuata kile anachosema na kutenda. Kimsingi kumfuata mtu ni kutenda na kuishi kile anachotenda na kuishi yule unayemfuata. Sisi ambao ni kondoo tunapaswa kumfuata Kristo mchungaji wetu: kutenda na kuishi kama alivyoishi Yeye, kufuata njia anayotuonesha. Dira yetu ya maisha inapaswa kuwa Kristo: kufuata maongozi yake. Kumfuata Kristo ni pamoja na kushika amri na mafundisho yake na kujidhatiti kumjua Kristo. Pili, tutazame namna Kristo Mchungaji Mwema anavyowatunza kondoo wake: _(i) Anawapatia uzima wa milele._ Uzima wa milele ni upi? Uzima wa milele ni kuishi pamoja na Mungu milele yote. Hivyo, wale wote wanaomwamini Kristo, wanaoisikia sauti yake na kumfuata wanapata uzima wa milele. _(ii) anawalinda ili adui asiwapore kutoka katika mikono yake._ Tukiwa chini ya mamlaka na ulinzi wa Kristo hatuwezi kushambuliwa na mporaji (yaani Shetani na mawakala wake). Tukikubali kuwa kondoo wa Kristo tunapata usalama wa roho na mwili. Hivyo, mwanadamu anapaswa daima kujifungamanisha na Kristo ili kuwa salama na kupata amani ya kweli.
Injili yetu ya leo inatufundisha mambo makubwa mawili: (1) Tunapaswa kuisikia sauti ya Kristo na kumfuata. Sauti ya Kristo si nyingine bali ni Neno la Mungu tunalohubiriwa. Kila mmoja ajiulize kama anasikiliza Neno la Mungu analohubiriwa. Kwa bahati mbaya watu wengi katika ulimwengu wa leo hawaoni umuhimu wa kuisikiliza sauti ya Kristo/Mungu inayosikika kwa njia ya Neno la Mungu. Wengi wetu tunapenda kusikiliza zaidi sauti za malimwengu na wachungaji wa uongo, tunasikiliza zaidi mitandao ya kijamii, tunasikiliza zaidi nyimbo zilizojaa tungo za ngono na matusi badala ya kujipa muda wa kusikiliza sauti ya Mungu/Kristo. Kadhalika, tunapaswa kumfuata Kristo. Kumfuata Kristo ni pamoja na kuwa tayari kupita njia aliyopita Yeye. Njia aliyopita Kristo ilihusisha mateso, kifo na ufufuko. Kwa bahati mbaya wengi wetu hatutaki kumfuata Yesu kwa kupita njia aliyopitia Yeye: _hatutaki mateso, hatutaki kufisha maisha ya dhambi na wala hatutaki kufufuka katika maisha mapya yenye kutufungamanisha na Kristo._ Hata hivyo, wengi wetu tumeingia katika imani ya Kikristo si kwa lengo la kumfuata Kristo Mchungaji wetu bali kwa lengo la kufuata wahubiri mashuhuri (yaani tunawafuata watu badala ya kumfuata Kristo), tunafuata utajiri, tunafuata miujiza, tunafuata pesa na maisha mazuri. Tubadilike. (2) Yesu ni Mungu sawa na Mungu Baba. Maneno ya Yesu, “Mimi na Baba tu umoja” yanathibitisha kuwa Yesu ni Mungu sawa na Mungu Baba. Hivyo kama Baba ni Mungu na Yesu ni Mungu pia maana ni umoja. Wayahudi walikwazika kwa maneno hayo na ndiyo maana waliokota mawe ili wampige Yesu kwa sababu “amejifanya Yeye mwenyewe kuwa ni Mungu” (Yn. 10:33). Maneno ya Yesu yanatukumbusha mojawapo ya maswali na majibu katika katekisimu ndogo ya Kanisa Katoliki: _Yesu ni nani? Yesu ni nafsi ya pili ya Mungu, ni Mungu halisi sawa na Baba._ Yesu ni Mungu. Je, ninajifungamanishaje na Yesu aliye Mungu kweli? Ipi nafsi ya Yesu katika maisha yangu? Majibu ya maswali haya yatufanye kumtambua zaidi Kristo, kumwamini na kujisalimisha kwake.
Leo ni Jumapili ya Miito. Tukumbuke kuombea kwa dhati miito mitakatifu na kwa namna ya pekee miito ya upadre na utawa maana mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Tuombee pia wito mtakatifu ya ndoa maana ndio wito mama.
MAOMBI YA MISA DOMINIKA YA 4 YA PASAKA(JUMAPILI YA YESU KRISTU MCHUNGAJI MWEMA)
Ndugu wapendwa,tunasikia sauti ya Yesu anayetuita kwa njia mbalimbali.Yesu anayetuita anatuumbia moyo wa kufahamu sauti yake.
Tuombe,
▪️Ee Bwana Yesu,uliahidi kutupa uzima wa kweli.Utuwezeshe kuthamini uhai wa kila mmoja kama zawadi ya thamani kubwa uliyotujalia.
▪️Ee Bwana Yesu, ulisema kwamba hakuna awezaye kutupokonya katika mikono yako.Ushike mikono yetu na kutuongoza,kama ulivyoishika mikono ya Petro aliyetaka kuzama baharini.
▪️Ee Bwana Yesu ulisema kwamba Baba ni mkubwa kupita vitu vyote.Utusaidie kutegemea zaidi msaada wa Mungu katika shida zetu
▪️Ee Bwana Yesu uliye mchungaji wetu:Usituache kamwe bali utuokoe katika hatari ya kujitenga nawe
▪️Ee Bwana Yesu,Uwe mwanga wetu katika giza la mashaka yetu,Uwe msaada katika shida,Uwe kimbilio katika hatari.
Ee Mungu Baba,tunakushukuru kwa njia ya Mwana wako aliyekuja kwetu awe kiongozi wetu katika mabonde ya shida na giza duniani hapa.Utusaidie tusiache kusikia sauti yake Bwana wetu anayeishi na kutawala pamoja na roho Mtakatifu daima na milele.......Amina.
#Powered by:-
KAJO MEDIA PRODUCTIONS
●KAJO ONLINE RADIOπ»
https://kajoonlineradio.wordpress.com
●KAJO ONLINE TVπΊ
https://youtube.com/channel/UCOHxrRXbGfaSRW7za3jcyhA
●KAJO MNJELU BLOGπ°
https://kajomnjelu.blogspot.com/?m=1

Comments
Post a Comment