WAZIRI BASHE AKIWASILISHA BAJETI WIZARA YA KILIMO 2022.



“Serikali ya Awamu ya Kwanza, ilitambua Tanzania kama nchi ya Wakulima na Wafanyakazi na kuwekeza katika kilimo hususani katika maeneo ya:- Vyuo vya Utafiti na Mafunzo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mashirika ya Umma yanayosimamia Kilimo, Bodi za Mazao na Vyama vya Ushirika.”

“Pia ilihamasisha kilimo na lishe kupitia programu na kampeni mbalimbali ikiwemo Ukulima wa Kisasa, Kilimo cha kufa na kupona, Chakula ni Uhai, Mtu ni Afya, Elimu ya Kujitegemea na Siasa ni Kilimo. Aidha, katika kipindi hicho, msisitizo uliwekwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kufikia kiwango cha kuongoza kimataifa kwa baadhi ya mazao ikiwemo korosho na mkonge”

“Serikali ya Awamu ya Pili, ilifanya mageuzi ya uchumi yaliyokuwa kichocheo katika maendeleo ya kilimo ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1983. Aidha, Serikali ilipunguza vikwazo katika biashara ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa ajili ya ustawi wa wananchi.”

“Serikali ya Awamu ya Tatu, iliimarisha Taasisi na kusimamia utawala bora, ilibinafsisha Mashirika ya Umma na Mashamba ya Umma, iliboresha Bodi za Mazao kwa kuzifanya Bodi hizo kuachana na biashara na badala yake kuwa Bodi za Udhibiti na Uendelezaji wa Mazao. Pia kwa kipekee iliunda Wizara ya Masoko na Ushirika na kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwa kuimarisha Serikali za Mitaa ambapo huduma za ugani za Kilimo na Mifugo zilihamishiwa TAMISEMI.”

“katika kuboresha maendeleo ya Sekta ya Kilimo, Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha na kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Kwanza (ASDP I), Programu ya Modenizesheni ya Ushirika, KILIMO KWANZA na SAGCOT. Pia, ilianzisha Benki ya Kilimo, Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo na taasisi mbalimbali ikiwemo Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Taasisi hizo zilianzishwa ili kuendeleza ufanisi wa kutoa huduma kwa wakulima katika upatikanaji wa pembejeo, miundombinu ya kilimo na ushirika.”

“Serikali ya Awamu ya Tano, ilianzisha na kutekeleza  Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Pia, iliboresha na kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara, reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege kwa lengo la kuchochea uwekezaji katika sekta za uzalishaji.”




“Serikali pia, ilihamasisha ukuaji wa uchumi unaotegemea maendeleo ya viwanda vya kusindika na kuchakata mazao ya kilimo (agro-processing) ikiwemo viwanda vya sukari, mafuta ya kula, pamba na nafaka.  Aidha, ilianzisha Mpango wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (Blueprint) na kutumia sera za kikodi kulinda viwanda vya mazao ya kimkakati yakiwemo sukari na mafuta ya kula”

“ukizingatia utekelezaji wa awamu zote tano, Serikali  za Awamu ya Kwanza na Awamu ya Nne, ziliwekeza katika msingi mkuu wa uzalishaji. Serikali za Awamu ya Pili na ya Tatu zilifanya kazi kubwa ya kufungua biashara na kuweka mifumo ya kitaasisi. Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu mbalimbali ambayo ni muhimu katika kuchochea uzalishaji, uongezaji wa thamani na usafirishaji.”

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhihirisha kwa vitendo utashi wa kisiasa kwa kutambua kuwa maendeleo ya uchumi yatatokana na sekta za uzalishaji hususan Sekta ya Kilimo. Azma hiyo itafikiwa kwa kuwekeza katika maeneo ya kimkakati ya utafiti, uzalishaji wa mbegu bora, uimarishaji wa huduma za ugani, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi wa mazao na uimarishaji wa upatikanaji masoko ya mazao ya kilimo.”

“katika kipindi cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imeongeza bajeti ya utafiti wa kilimo kutoka Shilingi Bilioni 7.35 hadi Shilingi Bilioni 11.63, huduma za ugani kutoka Shilingi Milioni 603 hadi Shilingi Bilioni 11.5, umwagiliaji kutoka Shilingi Bilioni 17.7 hadi Shilingi Bilioni 51.48 na uzalishaji wa mbegu kutoka Shilingi Bilioni 5.42 hadi Shilingi Bilioni 10.58.”

“Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza fedha za ununuzi wa nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kutoka Shilingi Bilioni 19 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi  Bilioni 119 mwaka 2021/2022. Hadi Aprili, 2022 fedha hizo zimewezesha ununuzi wa tani 183,045.384 za mpunga, mahindi na mtama ambazo zitauzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.”

“Serikali ya Awamu ya Sita imesimamia dhana ya kilimo ni biashara kwa kuimarisha mahusiano ya kimataifa ambayo yamefungua fursa ya masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Jitihada hizo zimewezesha kupatikana kwa fursa za masoko mapya ya mazao nje ya nchi ikiwemo soko la parachichi katika nchi za India na Afrika Kusini, ndizi nchini Kenya na mchele nchini Ubelgiji baada ya kukidhi viwango vya ubora. Aidha, tani 12,250 za zao la parachichi zenye thamani ya Shilingi Bilioni 24.95 ziliuzwa katika nchi mbalimbali”



“upatikanaji wa masoko umeongeza mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi ikiwemo mchele kutoka tani 184,521 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 176.49 mwaka 2020 hadi tani 441,908 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 476.8 mwaka 2021. Vilevile, mahindi kutoka tani 92,825 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 58.02 mwaka 2020 hadi tani 189,277 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 72.4 mwaka 2021 na parachichi kutoka tani 6,702 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 14.93 mwaka 2020 hadi tani 8,508 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 17.72 mwaka 2021.”

“Serikali imewezesha kupunguza riba za mikopo ya kilimo katika benki za biashara kutoka kati ya asilimia 17 na 20 hadi kufikia asilimia tisa (9). Punguzo hilo limewezesha wakulima kununua pembejeo kwa ajili ya uzalishaji, kuanzisha na kufufua viwanda vidogo ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.”
 
“Pia, Serikali imetoa ruzuku za pembejeo za kilimo kwa mazao ya korosho, tumbaku na pamba zenye thamani ya Shilingi Bilioni 178.84. Kadhalika, katika kipindi hicho Serikali imewezesha uundaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika na ununuzi wa magari 15, pikipiki 137 na kompyuta 82 kwa ajili ya kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika nchini. Jumla ya Shilingi Bilioni 2.44 zimetumika kuunda mfumo na kununua vitendea kazi hivyo.”

“mahitaji ya chakula kwa mwaka 2021/2022 yamefikia tani milioni 14.83 ambapo tani milioni 9.44 ni za nafaka na tani milioni 5.38 ni mazao yasiyo ya nafaka. Mahitaji hayo ukilinganisha na upatikanaji wa tani milioni 18.66 kwa mwaka 2021/2022, Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 126.”

Upatikanaji wa Mbolea

“Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu uzalishaji na uingizwaji wa mbolea nchini ambapo hadi Aprili, 2022 tani 436,452 za mbolea zimepatikana sawa na asilimia 63 ya mahitaji ya tani 698,260 ya msimu wa 2021/2022. Kati ya hizo, tani 274,973 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 43,579 zimezalishwa nchini na tani 117,900 ni bakaa ya msimu wa 2020/2021. Hadi Aprili, 2022 Bodi ya Tumbaku Tanzania kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika imesambaza mbolea NPK tani 20,689.9 na CAN tani 5,066.7 kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija..”

Upatikanaji wa Viuatilifu

“Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 upatikanaji wa viuatilifu vya udhibiti wa milipuko ya visumbufu vya mimea umefikia lita 106,000 vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.11. Hadi Aprili, 2022 jumla ya lita 34,817 za viuatilifu zimesambazwa kwa ajili ya kudhibiti nzi wa matunda na viwavijeshi.”




“Wizara imesambaza kwa wakulima tani 2,000 za mbegu za alizeti zenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.84 kwa utaratibu wa ruzuku. Mbegu hizo, zimesambazwa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu, Manyara na zinatarajiwa kuzalisha tani 400,000 za alizeti zitakazozalisha mafuta ya kula ya wastani wa tani 100,000.”
 
“Aidha, TARI imezalisha tani 37 za mbegu za ufuta na kusambaza tani 25 kwa wakulima na tani 18 za mbegu za karanga na kusambaza tani 15.5 kwa wakulima.”

“Wizara kupitia ASA, TARI, Bodi za chai, pamba, mkonge, korosho, pareto, kahawa na vikundi vya wakulima vimezalisha miche bora milioni 32.30 na mbegu tani 95,764 na kusambaza miche milioni 24.44 na mbegu tani 95,794 kwa wakulima. Aidha, Bodi ya Pamba Tanzania imesambaza tani 15,548 za mbegu za pamba kwa wakulima zinazotosha kupandwa katika hekta 621,920”

“Wizara imewezesha uanzishwaji wa mashamba darasa 695 kati ya hayo alizeti 378 na pamba 317. Vilevile, imeanzisha mashamba ya mfano 672 kati ya hayo alizeti  415 na pamba 257 katika mikoa ya Dodoma, Singida na Simiyu. Pia, maafisa ugani wa maeneo hayo wamepatiwa tani 10.5 za mbolea, viuatilifu (ekapack) 1,617 na viuagugu (ekapack) 1,584. Serikali imechukua hatua hiyo, ili kurahisisha utoaji wa mafunzo ya kilimo bora cha alizeti na pamba kwa vitendo.”

Katika mwaka 2021/2022 Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na ujenzi wa skimu sita (6) zenye ukubwa wa jumla ya hekta 9,349 katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Tabora, Mbeya na Manyara ambapo Shilingi Bilioni 12.06 zitatumika hadi kukamilika. Aidha, ukarabati wa skimu nane (8) zenye jumla ya hekta 3,711 katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Iringa, Katavi na Rukwa unaendelea ambapo jumla ya Shilingi milioni 917.5 zitatumika hadi kukamilika.
 
Aidha, taratibu za manunuzi zinaendelea kwa ajili ya ujenzi wa skimu nane (8) zenye jumla ya hekta 5,930 zilizopo katika mikoa ya Katavi, Ruvuma, Morogoro, Iringa, Simiyu, Mbeya na Tabora. Jumla ya Shilingi Bilioni 3.7 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa skimu hizo hadi kukamilika.




“Mheshimiwa Spika, eneo linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 695,045 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2021/2022. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 60.6 ya lengo la kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo 2025 kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025.”

Katika mwaka 2021/2022, tani 6,794 za singa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 21.8 na bidhaa mbalimbali za mkonge tani 711 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.14 zimeuzwa kwenye soko la ndani.
 
Aidha, tani 20,606.64 za singa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 33.77 na tani 866 za bidhaa mbalimbali za mkonge zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 2.46 zimeuzwa kwenye soko la nje. Vilevile, tani 73,028 za kahawa zenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Milioni 142.26 zimeuzwa kwenye soko la nje.

Kwa upande mwingine, tani 53,594.35 za soya zimeuzwa katika nchi za India, China, Rwanda na Kenya ikilinganishwa na tani 2,647 zilizouzwa msimu wa 2019/2020. Pia, tani 231,103 za korosho ghafi; tani 144,405 za pamba; tani 60,819 za kahawa; na tani 6,875 za kakao zimeuzwa kwenye soko la nje.

Ushiriki wa Sekta Binafsi katika Kilimo

Wizara imeendelea kuthamini mchango wa sekta binafsi kama kichocheo cha ukuaji wa Sekta ya Kilimo, usalama wa chakula, uongezaji wa thamani, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, kuongeza ajira na uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo. Taarifa ya Utekelezaji wa ASDP II kupitia sekta binafsi inaonesha kuwa kampuni 606 za sekta binafsi, Asasi za Kiraia 47 na Mashirika yasiyo ya Kiserikali 64 yamewekeza katika kilimo.

Aidha, Wizara imeratibu majukwaa 52 ya majadiliano na Sekta Binafsi kwa mazao ya asilia ya biashara, nafaka, mikunde, bustani na mbegu za mafuta ya kula kwa ajili ya kutatua changamoto za kikodi na kisera.




#BajetiKilimo2022
#Ajenda1030
#HusseinBashe

#Powered by:-
KAJO MEDIA PRODUCTIONS

Comments

Popular posts from this blog

HAYA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2021

MADA MEZANI on KAJO ONLINE RADIO