𝗝𝗘 𝗪𝗔𝗝𝗨𝗔 𝗞𝗨𝗣𝗜𝗚𝗔 𝗠𝗔𝗞𝗢𝗙𝗜 𝗡𝗔 𝗩𝗜𝗚𝗘𝗟𝗘𝗚𝗘𝗟𝗘 𝗪𝗔𝗞𝗔𝗧𝗜 𝗪𝗔 𝗛𝗢𝗠𝗜𝗟𝗜𝗔 𝗦𝗜𝗢 𝗨𝗧𝗔𝗥𝗔𝗧𝗜𝗕𝗨 𝗪𝗔 𝗟𝗜𝗧𝗨𝗥𝗝𝗜𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗔𝗡𝗜𝗦𝗔?
Mwandishi: FELIX, KALISTI J.
*TONE LA UPENDO*❤️❤️👇
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba, katika vita vya mafanikio, kuna njia nyingi mtu anapaswa azijue ili aweze kufanikiwa. Na mbinu mojawapo ya mafanikio, ni kumuiga yule aliyefanikiwa. Maana kutoka kwake, unaweza kujifunza vitu vingi vitakavyokusaidia katika safari yako ya maisha.
Kadhalika hata katika mambo ya imani, sio vibaya kwa Mkatoliki kumuiga Mkristo wa dhehebu lingine katika jambo jema analolifanya, lakini sio kila kitu unahitajika kukichukua kama kilivyo kutoka kwake. Mfano mzuri ni katika jambo hili la kupiga makofi na vigelegele Kanisani, hasa wakati ule ambao Padre anatoa homilia yake kwa Waamini.
Ukweli hata sasa kumekuwa na desturi baadhi ya Maparokia, wakati wa Misa Padre anapohubiri, utakuta Waamini wengi wakipiga makofi na vigelegele, kisa tu mahubiri hayo ya Padre yamewagusa na kuwafurahisha sana siku hiyo.
Na kibaya zaidi wengine utawasikia wakipiga makelele yao wakisema: 𝗡𝗱𝗶𝗼 𝗕𝗮𝗯𝗮, 𝗼𝗻𝗴𝗲𝘇𝗮 𝘀𝗮𝘂𝘁𝗶 𝗵𝘂𝗸𝘂 𝗻𝘆𝘂𝗺𝗮 𝗵𝗮𝘁𝘂𝘀𝗶𝗸𝗶𝗶, 𝘀𝗲𝗺𝗮 𝘁𝘂𝗽𝗼𝗻𝗲. Wakidhani kwamba wako sahihi kutokana na kuiga Ibada zinazofanywa na madhehebu mengine, kumbe wanakosea sana na wala utaratibu wa Liturjia yetu haisemi hivyo.
Katekisimu ya mafundisho ya Kanisa Katoliki yanasema kuwa: Wakati wa homilia, Waamini wote wanapaswa kukaa kimya na wala hawahitajiki kufanya chochote zaidi ya kusikiliza tu mahubiri ya Padre. Na hata baada ya mahubiri hayo kuisha, Kanisa linawasisitizia tena Waamini wake wakae hivyo hivyo katika hali ya ukimya, kwa lengo la kutafakari moyoni kile kilichohubiriwa na Padre, na sio kupiga makofi na vigelegele hata kama homilia ya Padre itawagusa vipi.
Kardinali Francis Arinze aliwahi kusema hivi: 𝗞𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗠𝗶𝘀𝗮 𝗵𝘂𝘄𝗮 𝗵𝗮𝘁𝘂𝗷𝗶 𝗸𝘄𝗮 𝗹𝗲𝗻𝗴𝗼 𝗹𝗮 𝗸𝘂𝗽𝗶𝗴𝗮 𝗺𝗮𝗸𝗼𝗳𝗶 𝗻𝗮 𝗸𝗶𝘀𝗵𝗮 𝗸𝘂𝗼𝗻𝗱𝗼𝗸𝗮 𝘇𝗲𝘁𝘂, 𝗯𝗮𝗹𝗶 𝘁𝘂𝗻𝗮𝗸𝘂𝗷𝗮 𝗸𝘄𝗮 𝗮𝗷𝗶𝗹𝗶 𝘆𝗮 𝗸𝘂𝗺𝘄𝗮𝗯𝘂𝗱𝘂 𝗠𝘂𝗻𝗴𝘂, 𝗸𝘂𝗺𝘀𝗵𝘂𝗸𝘂𝗿𝘂, 𝗸𝘂𝗺𝘄𝗼𝗺𝗯𝗮 𝗺𝘀𝗮𝗺𝗮𝗵𝗮 𝗷𝘂𝘂 𝘆𝗮 𝗺𝗮𝗸𝗼𝘀𝗮 𝘆𝗲𝘁𝘂 𝗻𝗮 𝘆𝗼𝘁𝗲 𝘁𝘂𝗻𝗮𝘆𝗼𝘆𝗮𝗵𝗶𝘁𝗮𝗷𝗶 𝗸𝘂𝘁𝗼𝗸𝗮 𝗸𝘄𝗮𝗸𝗲.
Hivyo Misa takatifu ni sadaka endelevu ya Kalvari, ambapo Yesu mwenyewe anamtolea Mungu Baba sadaka hiyo pale Altareni kwa mikono ya Padre, na sio sadaka ya kupiga makofi kama wengi wanavyofanya.
Na ndio maana Kanisa Katoliki baada ya kulitambua hili, wameamua kuweka utaratibu maalumu wa kupiga makofi wakati wa Misa na sio muda wote pale mtu anapojisikia. Mara nyingi makofi hupaswa kupigwa wakati Wanakwaya wanapoimba nyimbo za kumsifu Mungu, au wakati wa matangazo, Waamini huruhusiwa kupiga makofi kama kuna jambo muda huo limewafurahisha, lakini sio wakati wa homilia wala kipindi chote cha Kwaresma.
Katika hili naomba nieleweke wazi kuwa, sio vibaya kumpigia makofi Padre aliyetuongoza vema katika mahubiri yake, lakini makofi hayo yatakuwa na maana zaidi kama tungeyatumia makofi hayo kwa ajili ya kumsifu Mungu kwa uwezo ule aliompatia Padre kutuinjilisha, mwishoni kabisa mwa Misa hasa wakati wa matangazo tu na sio vinginevyo.
Kwahiyo nihitimishe kwa kusema kwamba, wakati wa Misa makofi na vigelegele yana muda wake kupigwa, na sio muda ule ambao Padre anahubiri.
𝗧𝗨𝗠𝗦𝗜𝗙𝗨 𝗬𝗘𝗦𝗨 𝗞𝗥𝗜𝗦𝗧𝗢...
Comments
Post a Comment